Wahukumiwa maisha jela kwa kujihusisha na dawa za kulevya

0
164

Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi (Mahakama ya Mafisadi), imewahukumu kifungo cha maisha jela Abdul Nsembo na mkewe Shamim Mwasha baada ya kutiwa hatiani kwa kosa ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin.

Aidha, mahakama hiyo imetoa amri ya kutaifisha mali za wawili hao, ikiwemo gari aina ya Discover 4 na dawa hizo zimetakiwa kuteketezwa.

Hukumu ya kesi hiyo namba 4 ya mwaka 2020, imetolewa na Jaji Elinaza Luvanda baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili kati ya Jamhuri na Utetezi na kujiridhisha kwamba Watuhumiwa wamekutwa na hatia katika makosa mawili ya usafirishaji dawa za Kulevya.

Wawili hao walishtakiwa Mei Mosi, 2019 baada ya kudaiwa kukutwa na Dawa za Kulevya aina ya Heroin wakiwa katika eneo la Mbezi Beach, Wilaya ya Kinondoni,Mkoani Dar es salaam, kinyume na sheria ya uhujumu uchumi.