Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza kuwa uchaguzi mdogo wa Ubunge katika jimbo la Muhambwe mkoani Kigoma utafanyika Mei 2 mwaka huu.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC Dkt Wilson Mahera imeeleza kuwa, Tume ilipokea barua kutoka Ofisi ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kutaarifiwa uwepo wa nafasi ya wazi wa kiti cha Ubunge katika jimbo hilo.
Amesema fomu za uchaguzi zitatolewa Machi 28 hadi April 3, kisha utafanyika uteuzi wa wagombea na kuanza kwa kampeni za uchaguzi Aprili 4 hadi Mei mosi.
Jimbo hilo la Muhambwe lililopo wilayani Kibondo, lipo wazi tangu Februari 12 mwaka huu kufuatia kifo cha Atashasta Nditiye.