Dkt. Kikwete: Dkt Magufuli alikuwa jembe langu

0
212

Rais Mstaafu wa awamu ya Nne wa Tanzania Dkt Jakaya Kiwete amesema katika uongozi wake, aliyekuwa Rais wa Tanzania Dkt John Magufuli alikuwa ni miongoni mwa Mawaziri aliowaamini na kuwatumani.

Amesema Dkt Magufuli alikuwa jembe,  ndio maana alikuwa akimteua kuwa Waziri katika wizara ambazo ni wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, wizara ya Mifugo pamoja na wizara ya Ujenzi.

Akizungumza wilayani Chato mkoani Geita wakati wa Misa Takatifu ya Mazishi ya Dkt Magufuli, Rais Mstaafu Kikwete amesema Dkt Magufuli alikuwa muadilifu, mchapakazi, mfuatiliji na asiyevumilia uzembe wakati wote wa uongozi wake.

Amesema kifo cha Dkt Magufuli kimemsikitisha sana kwa kuwa matarajio yake yalikuwa kiongozi huyo amalize muda wake wa uongozi salama ili apate nafasi ya kupumzika na kuifurahia nchi ambayo ameijenga kwa nguvu zake zote.

 Dkt Kikwete amesema Dkt Magufuli amefariki dunia akiwa na umri mdogo na akiwa tayari amefanya mambo makubwa kwa nchi yake na ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kumuombea ili apumzike kwa amani.

Aidha Dkt Kikwete amesema Rais Samia Suluhu Hassan ni kiongozi aliyepikwa na akapikika, hivyo ni dhahiri uongozi wake utawafuta machozi Watanzania.

Amemuhakikishia Rais Samia kuwa, Viongozi wote Wastaafu wapo tayari kushirikiana naye, hivyo awatumie kadri awezavyo.