Rais Filipe Nyusi wa Msumbiji amesema Dkt John Magufuli aliyekuwa Rais wa Tanzania, atakumbukwa kwa jinsi alivyohamasisha upendo na uchapakazi hata katika nchi jirani.
Akizungumza wakati wa hafla ya kitaifa ya kuaga mwili wa Dkt. Magufuli katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, Rais Nyusi amesema kuwa atamkumbuka Dkt. Magufuli kwa jinsi alivyokuwa akimpigia simu mapema asubuhi na kumwamsha akimwambia kuwa amkeni kwani ni muda wa kazi na hapa ni Kazi Tu, kitendo kinachoashiria alitaka kuona maendeleo hata katika nchi jirani.
Amesema nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) zitakumbuka upendo wa dhati aliokuwa nao Dkt. Magufuli aliyetaka kuona maendeleo yanakuwepo hata katika nchi hizo za kusini mwa Afrika.
Rais Nyusi amesema vilio vya Watanzania vinawakilisha vilio vya Waafrika wengine katika nchi za SADC, ambazo zimempoteza mwana wa Afrika, ambaye licha ya kufariki dunia lakini atabaki katika mioyo ya Watanzani na Waafrika wote.