Mwili wa aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Magufuli tayari umetolewa katika uwanja wa Uhuru mkoani Dar es salaam na kupelekwa hospitali ya Lugalo, baada ya kukamilika kwa shughuli ya kuaga kwa siku ya leo.
Mwili huo ulipelekwa katika uwanja huo majira ya asubuhi baada ya kufanyika kwa Misa ya kumuombea katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Petro lililopo Oysterbay.
Kwa mkoa wa Dar es salaam, shughuli ya kuaga mwili wa Dkt Magufuli itaendelea tena kesho kwa Wakazi wa mkoa wa Dar es salaam, na baadaye kusafirishwa kuelekea jijini Dodoma ambapo siku ya Jumatatu yatafanyika mazishi ya Kitaifa.
Dkt John Magufuli alifariki dunia.tarehe 17 mwezi huu mkoani Dar es salaam baada ya kuugua maradhi ya moyo.