Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa serikali imetoa kipaumbele kwenye matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika utendaji kazi wa shughuli za serikali za kila siku.
Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo jijini Dar es salaam wakati wa hafla ya utoaji tuzo za mashindano ya TEHAMA yaliyoandaliwa na kampuni ya HUAWEI upande wa Tanzania kupitia programu yake ya Seed of the Future.
Ametumia hafla hiyo kuwaonya watu wote wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii nchini na kuwataka Watanzania wote kutumia vizuri mitandao hiyo kwenye shughuli za maendeleo.
“Nawaonya watu wote wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii waache, ni vema wakatumia mitandao hiyo kwa kuhamasishana mambo mema zikiwemo shughuli mbalimbali za maendeleo, na kwa wataokiuka sheria ipo na inaendelea kufanya kazi,”amesisitiza Waziri Mkuu.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Majaliwa, matumizi ya TEHAMA yataongeza ufanisi katika kuwahudumia ipasavyo wananchi, mfano katika sekta ya elimu ambapo mwalimu mmoja anaweza kufundisha wanafunzi wengi kutoka katika shule tofauti kwa wakati mmoja.
Amesema kuwa serikali itaendelea kuwekeza katika kutengeneza mifumo ya TEHAMA ili kutekeleza kwa vitendo azma ya kuwapatia wananchi maendeleo hususani waishio maeneo ya vijijini huduma bora na kwa wakati.
Ameipongeza kampuni hiyo ya HUAWEI kwa uzinduzi wa program hiyo ya Seed of the Future ambayo inalengo la kuwajengea uwezo wa TEHAMA wanafunzi mbalimbali nchini katika hatua za awali.
Mashindano hayo ya TEHAMA ya HUAWEI yalianzishwa mwaka 2015 na baadaye mwaka 2016 yakazinduliwa Afrika Kusini, ambapo hadi kufikia mwaka 2017, wanafunzi Elfu 40 walikua wameshiriki.
Kwa upande wa Tanzania mashindano hayo yamezinduliwa mwaka huu, ambapo wanafunzi 500 walishiriki na baadaye kubaki 50.
Miongoni mwa wanafunzi hao 50, saba ndio waliokabidhiwa tuzo, na watatu kati yao wamepata fursa ya kushiriki hatua inayofuata ya mashindano hayo nchini Afrika Kusini.