Vitenge, kanga vyatandikwa barabarani kumuaga Dkt. Magufuli

0
466
Jeneza lenye mwili wa Dkt. John Magufuli likiwa ndani ya Kanisa Katoliki Parokia ya Mt. Petro mkoani Dar es Salaam wakati wa misa takatifu ya kuaga mwili huo.

Wakazi wa maeneo mbalimbali ya mkoa wa Dar es salaam wametandika kanga na vitenge pamoja na kutupa maua barabarani, wakati msafara uliobeba mwili wa Dkt. John Magufuli, aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ulipokuwa ukielekea Uwanja wa Uhuru.

Wakazi hao wamefanya hivyo ikiwa ni ishara ya kuonyesha huzuni zao kwa kuondokewa na Kiongozi wao na pia kumuaga kiongozi huyo.

Msafara huo uliobeba mwili wa Dkt. Magufuli ulikuwa ukitokea katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Petro lililopo Oysterbay baada ya kumalizika kwa Misa Takatifu ya kumuombea marehemu.

Msafara uliobeba mwili wa Dkt Magufuli umepita katika barabara mbalimbali ikiwa ni pamoja na Ali Hassan Mwinyi, Kawawa  kwenye maeneo ya Kinondoni, Magomeni na Ilala na barabara ya Kilwa.

Mamia ya wakazi wa maeneo hayo wameshindwa kuvumilia ambapo vilisikika vilio kutoka kila kona.

Shughuli inayoendelea hivi sasa ni Misa Takatifu ya kumuombea Dkt Magufuli inayofanyika katika uwanja huo, inayoongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es salaam, Jude Thadeus Ruwa’ichi.