TLP nao wamlilia Magufuli

0
273

Chama cha TLP kimeeleza kupokea kwa masikitiko kifo cha Dkt John Magufuli aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kuvitaka vyama vyote vya siasa kuweka pembeni tofauti zao katika kipindi hiki cha maombolezo.

Wakizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, – Augustino Mrema, Kaimu Mwenyekiti wa TLP Dominata Rwechungura na Katibu Mkuu wa chama hicho Richard Lyimo wamesema kifo cha Rais Magufuli ni pigo kwa Taifa.

“Sisi kama chama cha upinzani tunaamini Magufuli alikuwa Mwalimu na mfano mzuri wa kuigwa kiasi kwamba waliokuwa wakifanya naye kazi wamejifunza makubwa kutoka kwake”, wamesema viongozi hao.

TLP pia imetoa rai kwa Viongozi wa dini nchini kutumia kipindi hiki cha maombolezo kuliombea Taifa na kumkumbuka Dkt Magufuli kwa mazuri aliyoyafanya kwa Watanzania.

Aidha, chama hicho kimeelezea kufurahishwa na hatua ya kuapishwa kwa Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na na kuahidi kushirikiana naye kama ilivyokuwa kwa Dkt Magufuli.

“Tunaamini juu ya uwezo wa Rais aliyechukua hatamu Samia Suluhu Hassan kufuatia kifo cha Dkt .Magufuli na tutaendelea kumuunga mkono kama ilivyokuwa kwenye uchaguzi na tunaomba Watanzania wote kumpa ushirikiano katika kazi zake.” wameongeza viongozi hao wa TLP.