Man City yaendelea kushika usukani Ligi Kuu

0
1590

Ligi Kuu ya England imeendelea usiku wa Disemba Nne mwaka huu  kwa kuchezwa michezo minne ambapo Manchester City  wameendelea kushikilia usukani baada ya kuifunga timu ya Watford mabao mawili kwa moja.

Mabao  hayo mawili yamefungwa na Leroy Sane na Riyad Mahrez na kuiwezesha Man City kuendelea kuongoza ligi hiyo kwa alama tano mbele ya Liverpool yenye alama 36.

Watford wakiwa nafasi ya 11 na alama 20, walifunga goli la kufutia machozi katika dakika za lala salama kabla ya mchezo kumalizika.

Katika  uwanja wa London,  timu ya Westham United ikiwa nyumbani,  imeitandika Cardiff City mabao matatu kwa moja.

Mchezaji Lucas Perez aliyengia kipindi cha pili alifunga mabao mawili kwenye dakika za  49 na 54,  huku goli la tatu likifungwa na mchezaji Michail Antonio  katika dakika ya 61 na Cardiff City yenyewe ilipata goli moja kwenye dakika za nyongeza kabla ya mchezo kumalizika.

Katika mchezo mwingine, timu ya Brighton imeibuka na ushindi wa mabao matatu kwa moja dhidi ya Crystal Palace na AFC Bournemouth ikaitandika Huddersfield Town mabao mawili kwa moja.