Watanzania watakiwa kushiriki kuimarisha Utawala Bora

0
1759

Watanzania wametakiwa kushiriki katika kuimarisha Utawala Bora ili kutoa mchango wenye tija kwa maendeleo ya Taifa,  badala ya kuviachia jukumu hilo vyombo vinavyosimamia masuala ya utawala bora.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapteni Mstaafu George Mkuchika wakati akizindua maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za binadamu kitaifa jijini Dodoma.

Amesema kuwa ili kuwa na utawala bora nchini, watanzania wote wanahusika, kwa maana ya wale waliopewa dhamana ya kusimamia utawala bora na wananchi wa kawaida, kwa kuwa wenye dhamana ya kusimamia utawala bora wanahitaji ushirikiano kutoka kwa wananchi ili waweze kutekeleza majukumu yao kikamilifu.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuchika, Mtanzania wa kawaida anatakiwa abadilike kimtazamo na kifikra kuhusu uzingatiaji wa maadili, nidhamu ya kazi, vita dhidi ya rushwa, haki za binadamu, uwazi na uwajibikaji, na kusisitiza kuwa mabadiliko hayo ndio yawe  utamaduni wa mtanzania wa kila siku.

Naye, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt Mary Mwanjelwa ametoa wito kwa Watanzania kuwa wazalendo kwa kutanguliza maslahi ya umma kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.

Amesisitiza kuwa kupitia kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu ya mwaka huu inayosema kuwa  Udhibiti wa Mgongano wa Maslahi, Nguzo Muhimu Kujenga Utawala Bora, ni vema kwa kila Mtanzania akatanguliza maslahi ya umma mbele badala ya maslahi binafsi ili kufikia lengo la uchumi wa kati wa viwanda kama inavyohimizwa na Rais John Magufuli.

Kwa upande wake Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Jaji Mstaafu Harold Nsekela amesema kuwa maadhimisho ya siku ya maadili na haki za binadamu kitaifa ni muhimu kwa kuwa yanahimiza na kukumbusha kuzingatia misingi ya maadili, haki za binadamu, uwajibikaji, mapambano dhidi ya rushwa hasa kwa watumishi wa umma ambao jukumu lao kubwa ni kutoa huduma kwa wananchi.

Maadhimisho ya siku ya maadili na haki za binadamu kitaifa huratibiwa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali, Tume ya Utumishi wa Umma, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, lengo likiwa ni kuhamasisha uadilifu, uwazi, uwajibikaji na utawala bora nchini.