Jkt kulima hekari elfu 28 za mazao

0
173

Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) linatarajia kulima takribani ekari elfu 28 za mazao mchanganyiko ifikapo mwaka 2025 kutoka ekari zipatazo elfu 12 zilizolimwa kwenye msimu wa kilimo wa mwaka 2020/21.

Akizungumza katika ziara ya ukaguzi wa shughuli za kilimo kwenye kikosi cha jeshi cha MILUNDIKWA JKT, mkoani RUKWA, Mkuu wa JKT, Meja Jenerali CHARLES MBUGE amesema zitakapolimwa ekari hizo zitachangia kwa kiasi kikubwa kwa jeshi hilo kujitosheleza kwa chakula na kupata ziada ya kuchangia kwenye ghala la taifa

Meja Jenerali MBUGE amesema utekelezaji wa malengo hayo unakwenda sambamba na ujenzi wa viwanda kwenye baadhi ya vikosi ili kuongeza thamani ya mazao wanayolima na hatimaye kupata faida kubwa.

Mkuu huyo wa JKT amesema tayari jeshi hilo limejenga kiwanda cha kuchakata mahindi kwenye kikosi cha MLALE JKT kilichopo mkoani Ruvuma huku kikiendelea na ujenzi wa kiwanda cha kuchakata mpunga kwenye kikosi cha CHITA JKT cha mkoani Morogoro.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati Mkakati ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ndani ya JKT – Kanali HASSAN MABENA amesema kilimo cha mkakati kinachotekelezwa na JKT hakijaishia kulihakikishia chakula jeshi hilo, pia kimesaidia kubadili mtazamo wa wanajamii kwa jeshi.

Kanali MABENA amesema kabla ya mkakati huo, matarajio ya wanajamii hasa vijana waliokuwa wakijiunga na mafunzo ya jeshi yalikuwa kuajiriwa na jeshi, lakini mkakati wa kilimo umewasaidia kupata stadi za kazi ambazo zimewasaidia wengi kujikomboa kifkra na sasa wanawaza zaidi kujiajiri.