Wanawake Dar washauriwa kutumia fursa zinazowazunguka

0
237

Ikiwa bado ni mwezi wa tatu, siku chache baada ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, Mbunge wa Viti Maalum- Wanawake, Janeth Mahawanga amewasihi wanawake wanaoishi Dar es Salaam kujikwamua kiuchumi kwa kuzigeukia fursa kwenye maeneo yao.

Mahawanga ameyasema hayo leo mkoani Dar es Salaam wakati akizungumza na wanawake wa rika mbalimbali na kuhimiza wawe chachu ya kuziishi ndoto zao.

“ Ni muda wa kutumia vyema vile tulivyonavyo kwani wapo watu nje ya ‘Dar’ wanatamani wangepata nafasi kama hizi ili wakuze biashara zao,” ameeleza Mahawanga

Tafrija hiyo imetoa fursa pia kwa baadhi ya wanawake wanaopambana vyema kuzungumzia kazi zao. Huku historia ya mwanadada anayeendesha bajaji (Happiness Mosha) ikiufanya ukumbi kujawa na shangwe.

Mbali na kuzungumza juu ya fursa za kiuchumi wanawake wanazoweza kujikita nazo, Mahawanga amezindua Taasisi ya Tisha Mama yenye lengo la kusaidiwa wamama kudhubutu na kuwa wabunifu.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Godwin Gondwe amesema kuwa Mkuu wa Mkoa, Aboubakar Kunenge amewaamuru wakurugenzi wote wa Dar es Salaam kushirikiana na Tisha Mama ili kuhakikisha elimu ya kujikwamua kiuchumi inazidi kuenea.

Aidha, Kunenge amempongeza Mhawanga kwa kuwa mtu wa kuleta masuluhisho ya matatizo zaidi ya kulalamika.