Mkwamo wa Bandari ya Kisiju wapatiwa ufumbuzi

0
235

Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Elihuruma Lema amesema atatoa mashine za kuondoa kifusi cha mchanga kinachozuia maji kufika pwani ya Bahari ya Hindi, hivyo kuzorotesha shughuli katika Bandari ya Kisiju wilayani Mkuranga mkoani Pwani.

Lema amesema wataanza kutoa kifusi hicho na kuchimba njia ya maji kupita kufika bandarini kuanzia Aprili 2021, lakini pia wataanza mpango wa muda mrefu wa kuijenga bandari hiyo ili iweze kutumika muda wote bila kusubiria maji kujaa nyakati za usiku.

Ametoa ahadi hiyo mapema leo mara baada ya Mbunge wa Mkuranga, Abdallah Ulenga kumtaka aeleze mipango waliyonayo itakayowezesha bandari hiyo kutumika nyakati zote za mwaka.

Ulega ambaye pia ni Naibu Waziri wa Habari amezungumza na wananchi na kusema kuwa bandari ya Kisiju ndiyo bandari asili nchini, na imekuwa ikitumika kabla ya uhuru, hivyo ni wakati sasa wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kumaliza kero ambazo zimekuwa zikijitokeza kila mwaka katika kitega uchumi hicho.

Aidha, Ulega ameondoa zuio lililokuwa limewekwa na maafisa wa TPA kuwazuia baadhi ya wasafiri kutumia bandari ya Kisiju, wakiwataka kutumia bandari nyingine ikiwemo Nyamisati.

Katika hatua nyingine Ulega amemtaka meneja wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) kuomba kibali cha kukata miti iliyoota katikati ya bandari hivyo, hivyo kukwamisha maji kufika bandarini na vyombo vya usafiri kutoka na kuingia kwa urahisi.

Wananchi wamefurahia ziara ya mbunge wao kwani imekuwa ya mafanikio sana kwa kutatua kero hiyo ya bandari. Bandari hiyo mbali na kuwa tegemeo kwa wakazi wa Kisiju, inategemewa pia na wakazi wa visiwa vya Kware na Koma.