Kamati ya Bunge yaridhishwa na TBC

0
280

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Stanslaus Nyongo amesema kamati yake imeridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa jengo la studio za televisheni ya Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) linalojengwa Mikocheni mkoani Dar es salaam.

Kamati hiyo imefanya ziara ya siku mbili ambayo ilianzia Dodoma Machi 12 na kuhitimishwa Machi 13, 2021 Dar es salaam kwa kutembelea miradi iliyotekelezwa katika mwaka wa fedha 2020/2021 kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Mradi mwingine ni unaotekelezwa Makao Makuu ya TBC mkoani Dodoma ambao unahusisha ukarabati wa jengo la studio na ununuzi wa mitambo na vifaa vya redio jamii.

“Nimeridhika na maendeleo ya ujenzi wa jengo la TBC 2 linalojengwa hapa Mikocheni, wajumbe wa kamati yangu wameridhika na ujenzi wa mradi huu unaolenga kuboresha huduma ya utangazaji na utoaji wa habari za ukweli na uhakika kwa wananchi,” amesema Nyongo.

Katika majumuisho ya ziara hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Buyungu mkoani Kigoma, Aloyce Kamamba amesisitiza uongozi na watumishi wa shirika hilo kutunza majengo na kuwa na matumizi sahihi ya vifaa vilivyonunuliwa kwa ajili ya televisheni na redio ya Taifa na vitumike kama vilivyokusudiwa.

Naye Waziri wa Habari, Innocent Bashungwa ameishukuru kamati hiyo kwa kutembelea miradi hiyo na kusisitiza wizara yake itaendelea kutoa ushirikiano kwa kamati hiyo na imepokea maoni na ushauri waliotoa kwa TBC hatua inayoifanya shirika kuwa bora zaidi katika kuwapatia Watanzania haki yao ya Kikatiba ya kupata taarifa sahihi.