TBC kurusha matangazo ya mpira wa miguu

0
718

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa amesema kuwa wapo kwenye mchakato kuhakikisha kuwa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), linaweza kurusha matangazo ya michezo wa mpira wa miguu.

Bashungwa amedokeza hilo leo akijibu hoja za wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii ambayo imetembelea ofisi za TBC Dar es Salaam, kukagua ujenzi wa jengo la studio mpya na kujionea utendaji kazi wa shirika.

“TBC ukiangalia washindani wake wamefanya vizuri katika kufanya kutangaza michezo iwe ni mapato makubwa. Tayari tumeshaelekeza Katibu mkuu pamoja TBC twende kwenye muelekeo huo,” amesema Bashungwa.

Ameeleza kuwa hakuna sababu TBC ishindwe kuwa na king’amuzi chake na iweze kutangaza ligi mbalimbali kwani itaiwezesha pia kujiingizia mapato na itaacha kutegemea ruzuku za serikali.

Wajumbe wa kamati hiyo walisema kuwa ni wakati sasa TBC kuwa na haki ya kurusha matangazo ya mpira wa miguu nchini, na timu za taifa zinaposhiriki mashindano ya kimataifa kwani ni kituo cha umma, kinatazamwa na watu wengi zaidi nchini na pia hilo litasaidia kuongeza mapato.

Kwa upande wake mwenyekiti wa kamati hiyo, Stanslaus Nyongo amesema kuwa serikali imewekeza sana kwenye mazingira bora kuhakikisha shughuli za michezo zinafanyika nchini, hivyo haiwezekani yenyewe isifaidike kwa shughuli za kimichezo.

“Utangazaji na uoneshaji wa hizi ligi, tulitegemea TBC ambacho ni chombo cha serikali kineemeke. Haiwezekani infrastructure [miundombinu] ikawekwa na serikali halafu sisi tukazubaa kidogo kwenye kuvuna, akaja akavuna mtu mwingine,” ameeleza Nyongo.

Wakati huo huo, kamati hiyo imeipongeza TBC kwa mapinduzi makubwa ya upashanaji habari iliyofanya ambayo yameanza kuboresha mifumo ya urushaji matangazo na pia kuwapika waandishi na watangazaji ili wafanye kazi kwa weledi.