Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Lindi kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashitaka kuwafikisha mahakamani watuhumiwa watatu kwa tuhuma za kujipatia fedha shilingi milioni 92.6 kwa njia ya udanganyifu.
Watuhumiwa hao ambao ni Abdallah Mbinga, Mpimaji wa Ardhi (land surveyor) katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtama, Mohamed Mtungwe, Mjumbe wa Serikali ya Kijiji cha Nahukahuka B na Hassan Mohamed, Mkulima na mkazi wa kijiji cha Nahukahuka B wanadaiwa kutumia nyaraka za udanganyifu na kufanikiwa kujipatia fedha isivyo halali kinyume na sheria.
Watuhumiwa hao wanadaiwa kujipatia fedha zilizotolewa na kampuni Cassava Starch of Tanzania Limited kwa ajili ya kuwafidia wakulima wa kijiji cha Nahukahuka B kupisha mradi wa ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza wanga, ambapo mwekezaji huyo alikuwa ametoa fidia ya jumla ya shilingi milioni 450.34.
Kutokana na udanganyifu huo, mtuhumiwa wa kwanza alijipatia shilingi milioni 60.7, mtuhumiwa wa pili alijipatia shilingi milioni 10.05 na mtuhumiwa wa tatu alijipatia shilingi milioni 21.8.
Makosa matano yanayowakabili watuhumiwa hao ni kutumia nyaraka za uongo kwa lengo la kudanganya, kinyume na Kifungu cha 22 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya mwaka 2007, kula njama na kutenda kosa kinyume na kifungu cha 32 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya mwaka 2007 na kughushi nyaraka.
Aidha, makosa mengine ni kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, pamoja na uisababishia Serikali hasara.
Taasisi hiyo imewashukuru wadau wote kwa ushirikiano mkubwa wanaoendelea kuutoa ikiwepo kutoa taarifa mbalimbali za vitendo vya rushwa na pia imewataka watumishi kuendelea kuzingatia viapo vya utumishi na maadili ya kazi zao.