Wanaong’oa alama za upimaji ardhi waonywa

0
125

Serikali imewataka wamiliki wote wa ardhi ambao wamekuwa wakiharibu, kung’oa na kuhamisha alama za upimaji ardhi (Beacons) kuacha vitendo hivyo mara moja.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeeleza kuwa watakaobainika kufanya vitendo hivyo watachukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja kulipa faini ya shilingi Laki saba na nusu au kifungo cha mwaka mmoja jela, ama adhabu zote kwa pamoja.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ni kosa kisheria kufanya shughuli yoyote inayoweza kuharibu, kung’oa au kuhamisha alama za upimaji ardhi.

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imelazimika kutoa onyo hilo baada ya kubaini uwepo wa baadhi ya wananchi ambao wamekuwa wakiharibu, kung’oa na kuhamisha alama za upimaji ardhi, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Kufuatia kukithiri kwa vitendo hivyo katika maeneo mbalimbali nchini, wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imewaasa Watanzania wote kutojihusisha na vitendo hivyo kwa kuwa vinarudisha nyuma jitihada za serikali za kuongeza usalama wa umiliki wa ardhi kwa Wananchi wake.