Wagombea watatu wa Urais wa CAF wajiuzulu

0
289
Pichani waliokuwa wagombea Urais wa CAF, Augustine Senghor (kulia), Ahmed Yahya (kushoto), mgombea pekee wa Urais wa CAF (wa wapili toka kushoto) Patrice Motsepe, na Rais wa FIFA, Gianni Infantino.

Wagombea watatu wa Urais wa Shirikisho la Soka Afrika wamejitoa ili kumuunga mkono Patrice Motsepe wa Afrika Kusini, ambaye sasa anakuwa mgombea pekee wa nafasi hiyo.

Wa kwanza kujitoa alikuwa Augustin Senghor wa Senegal ambaye amesema amefanya hivyo kwa ajili ya maslahi ya soka la Afrika na kutangaza kuingia kwenye kambi ya Motsepe.

Jacques Anouma wa Ivory Coast kabla ya kujitoa alikutana na Rais wa nchi yake, Alassane Ouattara na baadaye akatangaza kukaa kando na kumuunga mkono Motsepe.

Ahmed Yahya wa Mauritania amekuwa wa mwisho kujitoa na kumuunga mkono mgombea huyo.

Kumekuwepo na tetesi kuwa kujiuzulu kwao kumeratibiwa na Rais wa FIFA, Gianni Infantino ambapo mapema wiki hii inadaiwa alikutana na wagombea hao wanne kwenye mkutano wa siri huko nchini Morocco.

Motsepe amebakia kuwa mgombea pekee, labda Rais wa sasa wa CAF, Ahmad Ahmad ashinde rufaa yake kwenye mahakama ya michezo ndiye anaweza kupambana naye kwenye uchaguzi wa Machi 12, 2021 utakaofanyika mjini Rabat, Morocco.