Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL) imesema kuwa inatarajia kuanza safari kwenda Guangzhou, China kuanzia Machi 20 mwaka huu kutokea jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi Mkuu wa ATCL, Ladislaus Matindi amesema kuwa safari hiyo ya China iliyokuwa ianze kuanzia Septemba 2020 imechelewa kutokana na janga la Virusi vya Corona.
“Tutakuwa tukisafiri mara moja kwa wiki, Jumamosi saa 11:00 alfajiri na kufika saa 3:00 usiku nchini China na tutarejea Tanzania muda huo huo Jumapili,” amesema Matindi akielezea safari hizo.
Amewataka wasafiri kuzingatia matakwa yote yaliyowekwa na serikali za pande zote ili kuweza kusafiri na kuingia katika nchi husika. Ameongeza kuwa tiketi zitauzwa tu kwa wale waliopimwa maambukizi ya COVID-19 na kutokuwa na maambukizi.