Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Mwinyi amewaapisha Mawaziri watatu aliowateua hapo jana kushika nyadhifa katika wizara tofauti za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mawaziri walioapishwa ni Saada Mkuya Salum anayekuwa Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Nassor Ahmed Mazrui anayekuwa Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia na Watoto pamoja na Omar Said Shaaban atakayeiongoza wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda.
Uteuzi wa Mawaziri hao umekamilisha idadi ya Mawaziri 16 wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar baada ya wizara hizo tatu kuwa wazi tangu Rais Mwinyi alipotangaza Baraza la Mawaziri kwa mara ya kwanza Novemba 19 mwaka 2020.
Rais Dkt Mwinyi pia amemuapisha Salum Yussuf Ali kuwa Kamishna wa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) baada ya kumteua Februari 10 mwaka huu.
Hafla ya kuwaapisha viongozi hao imefanyika Ikulu jijini Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Othman Masoud Othman, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdalla, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmeid Said pamoja na Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid.
