Wizara zatakiwa kuimarisha vitengo vya habari

0
230

Wizara za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimetakiwa kuviimarisha vitengo vyao vya habari,  ili kurahisisha mfumo wa kupokea malalamiko kutoka kwa Wananchi.
 
Rai hiyo imetolewa Ikulu jijini Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Mwinyi alipokutana na uongozi wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi pamoja na watendaji wa ofisi hiyo.
 
Dkt Mwinyi amesema ni vema pale Wananchi watakapoanza kutoa malalamiko yao wakawa wanapata majibu kwa uhakika kutoka Taasisi husika.
 
Amesisitiza haja ya kuwepo kwa mtu maalumu  atakayehusika na kazi ya kupokea malalamiko hayo kutoka kwa Wananchi,  ambaye atakuwa anayapeleka sehemu husika kufanyiwa kazi.
 
Rais Dkt Mwinyi amesema kuwa,  mfumo huo wa kupokea malalamiko kutoka kwa Wananchi utawasaidia kutatua kero zao na kusisitiza kwamba hatua zote zitakazokuwa zikiendelea yeye atakuwa akiziona.
 
Aidha, Rais Dkt Mwinyi amepongeza juhudi zinazofanywa na uongozi huo wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi katika kutekeleza maagizo aliyoyatoa.