Serengeti Boys yajiandaa kwenda Morocco

0
202
Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Gudila Swai akimpima shinikizo la damu mchezaji wa Serengeti Boys, Silverster Otto wakati wachezaji wa timu hiyo walipofika JKCI kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo kabla ya kushiriki mashindano ya kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON U17) yatakayofanyika nchini Morocco.

Wachezaji 24 wa Serengeti Boys wanaoshiriki mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana wa umri chini ya miaka 17 (AFCONU17) wamepimwa vipimo mbalimbali vya magonjwa ya moyo ikiwa ni sehemu ya matakwa ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).

Mtaalam kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Nuru Lugawa akimpima uzito na urefu mchezaji wa Serengeti Boys, Mohamed Mbarak wakati wachezaji wa timu hiyo walivyofika JKCI kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa afya ya moyo kabla ya kushiriki mashindano ya kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) yatakayofanyika nchini Morocco.

Upimwaji huo umefanyika katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ambapo endapo yeyote atakutwa na tatizo wataanza tiba mapema na kama hawa watafuata ushauri wa wataalamu wa afya jinsi ya kutunza mioyo yao.

JKCI ni hospitali pekee nchini iliyothibitishwa na CAF kuwa inakidhi vigezo vyote vya upimaji wa magonjwa ya moyo.

Fundi sanifu wa moyo (Cardiovascular technologist) wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Jasmin Keria akimpima mfumo wa umeme wa moyo unavyofanya kazi (Electrocardiography – ECG) nahodha wa Serengeti Boys, Ladaki Chasambi wakati timu hiyo ilipofika JKCI kwa ajili ya kuwafanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo kabla ya kushiriki mashindano ya kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) yatakayofanyika nchini Morocco.

Mbali na Tanzania, nchi nyingine zilizofuzu mashindano hayo ni Mali, Senegal, Ivory Coast, Nigeria, Zambia, Afrika Kusini, Uganda, Algeria, Morocco, Cameroon na Congo.

Tanzania ipo Kundi B pamoja na Congo, Nigeria na Algeria katika mashindano hayo yanayotarajiwa kufanyika nchini Morocco kuanzia Machi 13 hadi Machi 31 mwaka huu.