ACT-Wazalendo: Sharif kuendeleza yaliyoachwa na Maalim Seif

0
365

Chama cha ACT-Wazalendo kimepongeza uteuzi wa Othman Masoud Othman Sharif kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar na kueleza kuwa ni chaguo sahihi katika nafasi hiyo.

Katibu Mwenezi ACT-Wazalendo (Taifa), Salim Diman amesema huyo muda mfupi baada ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussien Mwinyi kufanya uteuzi huo uliokuwa ukingojewa kwa hamu na wakazi wa visiwa hivyo na Tanzania kwa ujumla.

Diman amesema chama hicho kinaamini kuwa Sharif ataendeleza yaliyoachwa na aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad ambaye alifariki dunia Februari 17 mwaka huu.

Kwa mujibu wa kifungu cha 40 (1) cha Katibu ya Zanzibar kama kilivyofanyiwa mabadiliko mwaka 2010 kinaendeleza kuwa endapo Makamu wa Kwanza wa Rais atafariki, mrithi wake anatakiwa kuteuliwa ndani ya siku 14 tangu kutokea kwa kifo hicho.

Taarifa ya Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Mhandisi Zena Said amesema uteuzi huo umeanza leo Machi 1, 2021 na mteule huyo ataapishwa Februari 2, 2021 Ikulu, Zanzibar.

Mapema leo asubuhi Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe alisema kuwa tayari chama hicho kilishawasilisha jina la mwanachama wake waliyempendekeza kurithi nafasi ya Maalim Seif.

Chama hicho kimesema Othman anakidhi matakwa ya chama na pia ni mhimili mzuri katika kuimarisha umoja wa kitaifa.