Sita kizimbani kwa madai ya kutakatisha bilioni 4

0
204

Wafanyabiashara sita wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na Kesi ya uhujumu Uchumi ikiwemo kosa la kutakatisha fedha zaidi ya shilingi bilioni 4.

Washitakiwa hao Baraka Madafu, Mark Mposo, Lusekelo Mbwele, Leena Joseph, Bernard Mndolwa na Salvina Karugaba wakazi wa Dar es Salaam wamefikishwa mahakamani hapo na kusomewa mashitaka 11.

Awali akiwasomea washitakiwa hao hati ya mashitaka Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon amedai kuwa katika tarehe tofauti kati Decemba 4, 2018 na Decemba 31 mwaka 2020 mshitakiwa Baraka Madafu na wenzake waliongoza genge la uhalifu nakujipatia zaidi shilingi bilioni 4 kutoka Benki ya NBC Tawi la Masaki Dar es Salaam kwa njia ya udanganyifu.

Katika shitaka la pili wanadaiwa katika tarehe tofauti kati ya Februari 6 mwaka 2019 maeneo ya Masaki washitakiwa hao walighushi nyaraka ya mkataba wa benki wakionesha kuwa watu 60 ambao ni waajiriwa wa Kampuni Peertech Limited ni wanufaika wa mkataba huo wakati wakijua sio kweli.

Shitaka la tatu hadi la 11 ambayo nayo ni ya kughushi nyaraka mawakili wa Serikali Paul Kadushi na Waknyo Simon wamesema washitakiwa hao katika tarehe tofauti mwaka 2019 na mwaka 2020 walighushi nyaraka ya kujipatia mkopo kupitia Benki ya NBC.

Baada ya washitakiwa kusomewa mashitaka yanayowakabili hawakuruhusiwa kujibu chochote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.

Hata hivyo wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi amedai upepelezi wa shauri hilo bado haujakamilika hivyo ameiomba mahakama kupanga tarehe nyingine kutajwa.

Kesi hiyo ya uhujumu Uchumi namba 13 ya Mwaka 2021 imeahirishwa hadi Machi 12 mwaka huu itakapotajwa na washitakiwa wamerudishwa rumande