JPM: WAANDISH WA HABARI KUWENI WAZALENDO

0
227

Rais Dkt. John Magufuli amewataka wananchi pamoja na waandishi wa habari kutanguliza maslahi ya Taifa.

Rais Magufuli ametoa rai hiyo wakati akihutubia wananchi waliojitokeza katika Uwanja wa Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam baada ya kuweka jiwe la msingi katika Soko Kuu la Kisutu na kuzindua Jengo la Jitegemee (Ofisi za Africa Media Group Limited) lenye vituo vya Channel Ten, Magic FM, Channel Ten Plus na Classic FM.

Kwa kusisitiza uzalendo, Rais Magufuli amesema si wanahabari pekee wenye uwezo wa kuchafua sifa ya nchi bali hata wananchi wengine wanaweza kufanya hayo kwa kutumia mitandao ya kijamii, huku madhara ya tabia hiyo yakiwa ni makubwa kwa Taifa.

Ameeleza kuwa kwa miaka mitano, serikali imeimarisha haki na wajibu wa vyombo vya habari ambapo usajili wa vyombo mbalimbali umeongezeka kufikia vituo vya redio 193, vituo vya TV 46, redio za mitandaoni 23 pamoja na magazeti na majarida 247.

Katika hatua nyingine amevitaka vyombo vya habari pamoja na taasisi za serikali kuwa wepesi kutoa taarifa za mbalimbali kwa wananchi hasa mambo ambayo serikali yao imekuwa ikiyafanya.

Kwa upande wake Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa amemshukuru Rais Magufuli kwa kuzindua kituo hicho cha habari na kwa kuendelea kuunga mkono wizara hiyo.

Bashungwa ametumia jukwaa hilo kuwashawishi wawekezaji wengine na Chama cha Mapinduzi ambacho ndiyo mmiliki wa Africa Media Group Limited kuwekeza pia kwenye sekta ya michezo kwani kina viwanja vingi katika maeneo mbalimbali nchini.