Rais Magufuli avunja Jiji la Dar es Salaam

0
197

Rais Dkt. John Magufuli kwa mamlaka aliyonayo ameivunja Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuanzia leo Februari 24, 2021.

Taarifa iliyotolewa na Waziri wa TAMISEMI, Selemani Jafo imeeleza kuwa Rais ameipandisha hadhi Halmashauri ya Manispaa ya Ilala kuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kianzia leo.

Uamuzi huo umekuja saa chache baada ya Rais Magufuli kutangaza nia ya kuvunja Jiji la Dar es Salaam wakati akihutubia wananchi kwenye hafla ya uzinduzi wa Daraja la Juu la Kijazi.

Katika hotuba hiyo alisema kuwa anavunja jiji hilo kwa sababu viongozi wake hawana eneo wanalowawakilisha wananchi licha ya kuwa hutengewe bajeti na posho, jambo ambalo si matumizi mazuri ya fedha za umma.

“Kuwa na madiwani ambao wanakaa hapa juu, wanachangiwa hela, hawana miradi ya maendeleo, wanakula posho na hawakuchaguliwa na watu, hili nitalikata,” ameeleza Dkt. Magufuli.

Katika taarifa yake, Waziri Jafo amesema kuwa waliokuwa watumishi wa halmashauri ya jiji iliyovunjwa watapangiwa vituo vipya vya kazi na pia taratibu za kuhamisha shughuli za halmashauri iliyovunjwa kwenda halmashauri mpya ya jiji zinaendelea.