Simba yaendeleza ubabe Klabu Bingwa Afrika

0
191

Wawakilishi pekee ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, ya Simba imezidi kujichimbia kileleni mwa msimamo wa Kundi A katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika hatua ya makundi baada ya kuwachapa bao 1-0 mabingwa watetezi Al Ahly kutoka Misri, mechi iliyopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Simba ilipata bao la ushindi kupitia kwa winga hatari kutoka Msumbiji, Luis Miquissone dakika ya 39 kwa shuti kali lililomshinda mlinda mlango wa Al Ahly na kutinga nyavuni.

Matokeo mengine ya kundi hilo, Al-Merreikh ya Sudan imezidi kuzama baada ya kukubali kichapo cha pili mfululizo kwa kufungwa nyumbani mabao 4-1 na wageni AS Vita Club ya DR Congo ambao walipoteza mechi ya kwanza nyumbani kwa kufungwa na Simba bao 1-0.

Kwa matokeo hayo Simba wamefikisha alama 6 na kuongoza huku nafasi ya pili ikishikwa na AS Vita yenye alama 3 sawa na Al Ahly wenaoshika nafasi ya tatu. Al-Merreikh wanaburuza mkia wakiwa na hawana alama baada ya kupoteza michezo yote miwili.

Kwingineko chama la Simon Msuva timu ya Wydad Casablanca imepata ushindi wa ugenini kwa kuwafunga wenyeji Petro Atletico ya Angola bao 1-0 lililofungwa na Ayoub El Kaabi dakika ya 71, mchezo wa Kundi C.