Tanzania yatupwa nje ya fainali za AFCONU20

0
233

Timu ya Taifa ya Tanzania chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes, imeaga rasmi fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 20 baada ya kula mweleka wa mabao matatu kwa bila dhidi ya Morocco.

Kipigo hicho si tu kinaiondoa Tanzania katika mashindano hayo ya Afrika lakini pia kinazima kabisa ndoto zake za kufuzu fainali za kombe la FIFA la Dunia kwa vijana chini ya umri wa miaka 20.

Morocco inaungana na Gambia na Ghana kusonga mbele katika hatua ya robo fainali ya AFCONU20 kutoka Kundi C.

Katika michezo mitatu ya hatua ya makundi, Ngorongoro Heroes wametoka sare mchezo mmoja dhidi ya Gambi (1-1) na kufungwa michezo miwili dhidi ya Ghana (4-0) na Morocco (3-0).

Timu pekee kutoka ukanda wa Afrika Mashariki iliyopiga hatua katika robo fainali ya mashindano haya ni Uganda, The Hippos, kufuatia kuwanyuka wenyeji Mauritania mabao mawili kwa moja katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi.

Ushindi huo umeiwezesha Uganda kumaliza katika nafasi ya pili nyuma ya Cameroon katika Kundi A.