Mtumishi wa TANESCO kizimbani kwa uhujumu uchumi

0
294

Afisa Ugavi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Clemency Mlay amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam akikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi ikiwemo kosa la kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya shilingi milioni 800.

Mshitakiwa Mlay amefikishwa mahakamani hapo na kusomewa mashitaka yake na Wakili wa Serikali Mkuu, Martenus Marando mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Rashid Chaungu.

Wakili Marando amesema Mlay akiwa mtumishi wa umma alitenda makosa hayo katika tarehe tofauti, Julai 2018 na Juni 2019, kwenye eneo la bohari ya kupokea na kutunza vifaa vya umeme vya TANESCO iliyopo Kurasini jijini Dar es Salaam.

Aidha, Wakili Marando amesema mshitakiwa huyo alihusika katika wizi na upotevu wa vifaa mbalimbali vya umeme wakati akitekeleza majukumu yake ya kupokea na kuhifadhi vifaa kama mtumishi wa umma hivyo kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya shilingi milioni 800.

Hata hivyo baada ya mshitakiwa kusomewa mashitaka yanayomkabili, hakuruhusiwa kujibu chochote mahakamani hapo kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.

Hakimu Chaungu ameahirisha kesi hiyo hadi Machi 8, 2021 kwa ajili ya kutajwa na mshitakiwa amerudishwa rumande.