Rais Magufuli: Tuendelee kumuomba Mungu atuepushe na magonjwa

0
190

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli amewataka Watanzania kuendelea kumuomba Mungu aliepushe Taifa dhidi ya Ugonjwa wa Corona na kusisitiza kuwa hatatangaza Lockdown.

Rais Magufuli ameyasema hayo wakati akiongoza waombolezaji kuuaga mwili wa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi kwenye viwanja vya Karimjee jijini Dar es salaam leo Ijumaa Februari 19, 2021.

“Tusitishane na kuogopeshana Mungu yupo, Mungu ndiyo muweza wa yote. Tuendelee kusimama na Mungu, tulishiinda Corona mwaka jana. Naomba Tusimame na Mungu,” amesema Rais Magufuli.

“Magonjwa yapo na yataendelea kuwepo, magonjwa ya vifua, magonjwa ya kupumua yapo. Kufa tutakufa tu, unaweza ukafa kwa malaria, cancer [saratani] na magonjwa mengine, kufa kupo, ila kamwe tusimuache Mungu. Waislamu walitangaza muda wao wa kuomba, Waislamu wameanza leo, kesho Wasabato, Jumapili Wakristo kwa siku 3 kwa kuomba na kufunga tutashinda,” ameongeza Rais Magufuli.

Amewaomba Watanzania kumuomba Mungu kama kuna mahali wametetereka kwani Mungu ndiyo mwenye uwezo wa kila kitu.

“Viongozi wa dini endeleeni kusisitiza maombi, tumeshinda mwaka jana na sasa naomba tuendelee kumuomba Mungu.” amesema.

“Hatutaweka Lockdown kwa sababu Mungu muda wote yupo.Taifa hili lipo mikononi mwa Mungu na Mungu ataendelea kusimama nasi.

“Natoa pole kwa Watanzania wote kwa vifo vyote viwili, cha Maalim Seif pamoja na cha Balozi Kijazi, Jana nilimtuma Makamu wa Rais na Dkt. Bashiru waniwakilishe kwenye mazishi ya Maalim Seif,” ameongeza kiongozi huyo.

Katika hatua nyingine Rais Magufuli amesitikitishwa na watu wanaozusha taarifa za uongo kwamba Waziri wa Fedha, Dk. Philip Mpango amefariki dunia huku akisoma SMS aliyotumiwa na Dk. Mpango kuhusu hali anayoendelea nayo.