Rais Dkt. Mwinyi aomboleza kifo cha Dkt. Muhammed Khatib

0
351

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ametuma salamu za rambirambi kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki kufuatia kifo cha Dkt. Muhammed Seif Khatib aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Kiswahili la Zanzibar pamoja na Mjumbe wa Kamisheni ya Utumishi wa Umma.

Dkt. Khatib amefariki leo (Februari 15, 2021) katika Hospitali ya Al-Rahma, Zanzibar na anatarajiwa kuzikwa kesho saa nne huko kijijini kwao Umbuji, Jimbo la Uzini, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.

Katika salamu hizo za rambirambi, Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa amepokea kwa mshtuko na huzuni kubwa taarifa ya kifo cha Dkt. Khatib.

“Mimi namfahamu Dkt. Khatib kuwa ni kiongozi mahiri, aliyependa kazi, mvumilivu na aliyekuwa na mashirikiano mazuri na wenzake wote ndani ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,” imeeleza sehemu ya salamu hizo za rambirambi.

Aidha, kupitia salamu hizo za rambirambi, Rais Dkt. Mwinyi amemuomba Mwenyezi Mungu kuwapa moyo wa subira na uvumilivu katika kipindi hichi kigumu cha msiba, familia, marafiki, ndugu pamoja na wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla.