Serikali: Vibali vya kuagiza sukari nje ya nchi mwisho 2022

0
195

Waziri wa Kilimo, Profesa Adof Mkenda ametoa onyo kwa makampuni ya uzalishaji sukari kuwa serikali haitatoa vibali vya kuagiza sukari nje ya nchi ifikapo mwaka 2022 na hivyo kuvitaka viwanda hivyo kuongeze kasi ya uchakataji wa miwa ya wakulima na kuzalisha sukari ya kutosha.

Profesa Mkenda ametoa kauli hiyo leo wakati akiongea na uongozi wa mkoa wa Morogoro akiwa ziarani kukagua hali ya uzalishaji sukari katika viwanda vilivyopo mkoani humo na pia kukutana na wakulima wadogo wa miwa.

“Shida yetu ya sukari haitokani na kukosa miwa bali ni uwezo mdogo wa viwanda kuchakata miwa yote ya wakulima nchini hali inayosababisha baadhi ya miwa ya wakulima kukosa soko,” amesema Waziri Mkenda.

Amebainisha kuwa wizara ya kilimo ina mkakati wa kuhakikisha miwa yote ya wakulima inachakatwa na viwanda vilivyopo ili kuondoa tatizo la upungufu wa sukari na kuwa utaratibu wa sasa viwanda kupewa vibali vya kuagiza sukari nje hauna manufaa kwa taifa.

“Mwaka huu vibali vya kuagiza sukari itakayopungua itatolewa kwa makampuni kwa utaratibu wa kawaida lakini ifikapo mwaka 2022 hakutakuwa na vibali vya viwanda na ikilazimu basi Bodi ya Sukari ndio itapewa kibali cha kuagiza sukari itakayopungua,” amesisitiza Prof Mkenda

Naye Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Emanuel Kalobero amesema mkoa huo una viwanda vitatu vya kuzalisha sukari lakini bado uzalishaji wake ni mdogo hali inayopelekea miwa ya wakulima kukosa soko na kuharibika.