Serikali yaingilia sakata la Namungo FC kushikiliwa Angola

0
404

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania inaendelea kufuatilia sakata la wachezaji na maofisa wa Klabu ya Namungo kushikiliwa na jeshi la Angola ilikokwenda kwa ajili ya kushiriki mchezo.

Akitoa hotuba ya kuahirisha Mkutano wa 12 wa Bunge, amesema kuwa jambo hilo ni siasa za kwenye michezo na kwamba serikali inaendelea kulishughulia ili timu hiyo icheze mchezo wake na irejee nyumbani salama.

“… timu hiyo mpaka sasa inashikiliwa na jeshi la nchi ya Angola ikiwa ni siasa za kwenye michezo. Sisi kama Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje tunalifanyia kazi jambo hilo,” amesema Waziri Mkuu.

Aidha, ameitakia heri timu hiyo katika mchezo wake ambapo itashuka dimbani Februari 14, 2021 kukabiliana na 1º de Agosto katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika.