Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti ya Kuondoa Umaskini Nchini (REPOA) Dkt Donard Mmary amesema kuwa matokeo ya utafiti ndio yanayoweza kusaidia kuandaa sera na mipango ya kuleta maendeleo kwa haraka kwa wananchi na Taifa ikiwemo kufikia uchumi wa viwanda.
Dkt Mmary ametoa kauli hiyo mjini Morogoro mara baada ya ufunguzi wa mafunzo ya siku tano, yanayoshirikisha watendaji wa ngazi ya kati wa serikali wanaohusika na mipango pamoja na sera.
Lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo washiriki wa namna ya kutumia matokeo ya tafiti mbalimbali zinazofanywa na wataalamu wa kiuchumi ili kuharakisha maendeleo ya Taifa.
Dkt Mmari ameongeza kuwa kwa sasa tafiti nyingi zinazofanywa na wataalamu wa kiuchumi wazawa zimekuwa na faida kubwa kwa kuwa zimekua zikitumika katika kuharakisha maendeleo .