Changamoto za manunuzi ya vifurushi vya mitandao ya simu pamoja na muda wa matumizi zitapata suluhisho ifikapo Februari 28, 2021.
Akizungumza na TBC ARIDHIO Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile amesema wizara inashughulikia changamoto hiyo ili kuja na suluhisho la kudumu.
“Sisi kama wizara tumedhamiria kabisa kuhakikisha tunalitatua hili jambo lakini linahitaji umakini, kwa hiyo kupitia TCRA [Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania] tunashirikisha wadau ikiwa ni pamoja na makampuni ya simu na wadau mbalimbali kupata maoni yao, lakini tunatarajia ifikapo mwisho wa mwezi huu tutakuwa tumepata majibu ya kudumu…,” amesema Dkt. Ndugulile.
Pia, Ndugulile amesema wizara imejipanga kupambana na uhalifu wa kimtandao kwa watu wanaotumia mitandao ya simu kufanya utapeli na wanaotumia mitandao kukashifu watu wengine.
“Tunataka twende mbali zaidi kupambana na uhalifu wa kimtandao, watu ambao wanatumia njia ya utapeli kupata hela kutoka kwa watu wengine lakini hata wale ambao wanatumia mitandao ya simu kukashifu watu wengine, kwa hiyo tunataka tuje na mikakati kama serikali kudhibiti…,” ameongeza Ndugulile.