Maafisa habari watakiwa kuielezea miradi ya maendeleo kwa wananchi

0
296

Washitiri (maafisa habari) wanaoshiriki mafunzo ya watoa elimu kwa umma wametakiwa kuwa chachu ya kuwahabarisha wananchi juu ya mengi mazuri yanayofanywa na Serikali.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa wakati akifungua mafunzo hayo mikoani Morogoro na kuongeza kuwa maafisa hao wanawajibu wa kuujulisha umma juu ya maendeleo yanayofanywa na Serikali ikiwepo miradi ya kimkakati.


Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo – Innocent Bashungwa

Aidha, ameagiza taasisi na mashirika yote yaliyotakiwa kuleta maafisa habari wao na hawajajitokeza kwenye mafunzo hayo kuwa na maelezo ya kina ili kujua changamoto zilizokwamisha wao kufika.

“Nataka kujua sababu za maofisa habari waliotakiwa kuhudhuria mkutano huu na hawajaja, haiwezekani mkutano muhimu kama huu halafu watu wasije wakati Serikali inawategemea kwenye kupata mafunzo ili wawajulishe wananchi juu ya kazi za taasisi na wizara zao,” Waziri Bashungwa amesisitiza.

Kwa upande wake Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi amesema ni wajibu wa kila afisa habari kuwatumikia wananchi.


Msemaji Mkuu wa Serikali – Dkt. Hassan Abbasi

“Ni haki na wajibu wa afisa habari kutoa taarifa kwa wananchi pale zinapohitajika kufanyika, lakini kuna maafisa hawapokei wala kujibu messages [jumbe] za wananchi wanapokuwa wanahitaji ufafanuzi wa jambo kwenye taasisi zao. Jamani niwakumbushe kuwa nafasi tulizonazo ni wajibu wetu kuwahudumia Watanzania muda wote.”

Mkurugenzi Mkuu wa Shirikisha la Utangazaji Tanzania (TBC), Dkt. Ayub Rioba Chacha amesema mikutano ya aina hii imekuwa na matokeo chanya tangu kuanzishwa kwake na sasa mipango iliyopo ni kuboresha huduma za uhabarishaji kupitia teknolojia hasa kupitia mitandao ya kijamii.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) – Dkt. Ayub Rioba Chacha

“Huu ni mkutano wa 104 kuwakutanisha maafisa habari na wadau wa elimu kwa umma, pamoja na mengi watakayojifunza kwenye mkutano huu, ni matumizi ya mitandao ya kijamii kuwahabarisha wananchi juu ya yanayoendelea kwenye taasisi zao,” ameeleza Dkt. Rioba.

Leo ni siku ya pili ya mkutano huo wa siku tano ambao kaulimbiu yake ni “Dhima ya Mawasiliano Kwenye Kuhabarisha na Kushirikisha Wananchi Katika Maendeleo ya Uchumi wa Kati Yenye Sura ya Utu.”