Bilioni 5 kupeleka huduma ya saratani Kanda ya Ziwa

0
307

Serikali imetenga shilingi bilioni 1 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la huduma za Saratani lenye katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando ili kuweza kusogeza huduma za saratani kwenye mikoa nane ya Kanda ya Ziwa .

Waziri wa Afya, Dkt. Dorothy Gwajima amesema jengo hilo ambalo litagharimu shilingi bilioni 5.4 litasaidia kupanua huduma za saratani nchini na kuwapunguzia muda wakazi wa kanda hiyo ambapo awali huduma hizo zilikua zikipatikana jijini Dar es Salaam kwenye Taasisi ya Saratani ya Ocean Road na hivyo kudidimiza uchumi wa wana familia wengi.

“Dhamira ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli ni kuimarisha huduma za afya kwenye maeneo mengi nchini hususani kuboresha huduma za Saratani kwenye hospitali za rufaa za kanda ili kuhakikisha anawapunguzia kero za kufuata huduma hizi jijini Dar es salaam ikiwa ni pamoja na kudhibiti ugonjwa huu kwa kufuata mtindo bora wa maisha,” amesema Dkt. Gwajima.

Dkt. Gwajima ametoa elimu kwa wananchi waliofika kwenye viwanja vya hospitali hiyo kwa ajili ya uchunguzi wa saratani ambapo amewataka kudhibiti magonjwa hayo kwa kubadilisha mtindo wa maisha, kufanya mazoezi, kutokuvuta sigara, kunywa maji mengi, kutokunywa pombe kupitiliza na uzito mkubwa.

“Wananchi lazima waelewe na kuwa na mfumo mzuri wa maisha kwa kufuata mtindo bora wa maisha na kujenga mazoea ya kwenda kwenye vituo vya afya kufanya uchunguzi wa afya zetu ili endapo upo kwenye hatua ya awali uweze kutibiwa mapema na kuishi maisha yako ya kawaida, ila ukichelewa itaenda kwenye hatua ya tatu na ya nne ambayo ni ngumu kuzuilika.”

Ameongeza kuwa magonjwa yasiyo ambukiza kama presha, moyo, kisukari na mengine yanaweza kuzuilika kwani Mwenyezi Mungu amewapa maarifa watu wake hivyo kila mmoja anatakiwa kutekeleza yale yote wanayoelekezwa na wataalam kwa kuwa siri ya kudhibiti magonjwa yapo kwenye maarifa ambayo yalitolewa na mababu kwa kutumia tiba asili.