JPM apigilia msumari utumiaji wa dawa za asili

0
249

Rais Dkt. John Magufuli ameendelea kusisitiza utumiaji wa dawa za asili katika kujikinga na maambukizi ya magonjwa mablimbali ikiwemo maambukizi ya virusi vya corona.

Dkt. Magufuli ameyasema hayo jijini Dodoma katika uzinduzi wa makao makuu mapya ya Jeshi la Magereza yaliyopo Msalato na kusisitiza kuwa hakuna linaloshindikishana ukimtanguliza Mungu katika maombi, hivyo amewaomba viongozi wa dini kuendelea kuhamasisha wananchi kuomba ili janga la corona liondoke.

“Siku zote Mungu ni mshindi wa kila jambo tutakalokuwa tunamuomba, sisi Tanzania tayari tumeshashinda mbele ya Mungu kwa sababu tunamtegemea Mungu, hakuna kitakashondikana, tuendelee kuchukua tahadhari, ” amesema Dkt. Magufuli.

Amesema zipo dawa nyingi za kujifukiza, ambazo zimethibitishwa na wizara ya afya kwa ajili ya matumizi ya binadamu na zinasaidia kujikinga na maradhi mbalimbali.

“…Kuna dawa inaitwa COVIDOL zinafanya kazi kwa sababu zimekuwa proved [zimethibitishwa] na mkemia mkuu, na zile zinaleta reaction [matokeo] ya ku-affect [kuathiri] kwenye virus [virusi] na bakteria kwa asilimia 99, mimi nawaeleza ukweli…,” amesisitiza Dkt. Magufuli.

Aidha, ametoa wito kwa taasisi zinazosimamia dawa za asili waziendeleze kwani ni wakati sahihi wa kutumia dawa za asili katika kupambana na maradhi.

“Madawa haya yalipigwa vita na wakoloni kwa sababu ya uchumi ukiwa na mti wako hata kama unaponesha malaria utaambiwa huu ni mti wa kishamba, na sisi tulikubali kwa sababu tuliona hao wanaotutawala wanajua kila kitu,” ameongeza Dkt. Magufuli.