TCRA yatoa sababu kusitisha usajili Online TV na blogs

0
250

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imefafanua kuwa wamelazimika kusitisha utoaji leseni mpya kwa watoa maudhui kwa njia ya mtandao (Online TV na blogs) kwa lengo la kufanya tathmini ya kimaudhui kutokana na ongezeko la vyombo hivyo kila mwaka na ukiukwaji wa maadili na kanuni.

Kwa Mujibu wa TCRA tangu kuanza kutumika kwa Sheria ya Mawasiliano ya Kieletroniki na Posta ya Mwaka 2018 ambayo iliwalazimu watoa maudhui mtandao kusajiliwa kabla ya kutoa huduma hiyo kumekuwepo na ongezeko kubwa ambapo tangu 2018- 2021 online TV 432 zimesajiliwa.

Mkuu wa Kitengo cha Leseni za Mawasiliano TCRA, Mhandisi Andrew Kisaka ameeleza kuwa ongezeko hilo ni kwa kila mwaka ambapo mwaka 2020 umeandika rekodi ya usajili wa online TV 211 ikiwa ni mara tatu ya online TV zilizosajiliwa 2018 ambazo zilikuwa 57, huku kwa mwaka 2019 ongezeko la online TV likiwa mara dufu kwa kufika 159 kutoka 57 za mwaka 2018.

Kasi hiyo ya usajili wa online TV ilianza kuonekana pia kwa mwaka huu 2021 ambapo kabla yay a kusitishwa kwa zoezi hilo la usajili ndani ya siku 28 za mwezi Januari jumla ya online TV 5 zimesajiliwa kasi ambayo pia imepelekea kuonekena kwa ukiukwaji wa maadili pamoja na kanuni za maudhui mtandao

Ongezeko hili limefanya mamlaka hiyo kusitisha utoaji leseni kuanzia Januari 2021 mpaka Juni 30, 2021.

Deodatus Balile Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri nchini (TEF) anakiri ni kweli maudhui ya mtandaoni yanaukakasi kwa jamii na kutoa wito kwa TCRA kutoa elimu zaidi badala ya kutengeneza kanuni nyingine.

Kwa upande wake Christopher Minyaro ambaye ni mkazi wa Dar es Salaam amesema kuwa TV na blogs hizo zimekuwa zikipotosha kwani mara nyingi kinachoandikwa, na kilichomo ndani ya video, haviendani, hivyo kuvifanya visiaminike.