Wanne kizimbani kwa uhujumu uchumi

0
265

Watu wanne wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es salaam, wakikabiliwa na Kesi ya uhujumu uchumi ikiwemo kosa la kukutwa na nyara za Serikali zenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni arobaini na tano.

Washitakiwa hao Idd Selemani, Maria Mole, Abubakar Sauka pamoja na Hassan Salum wamefikishwa Mahakamani hapo na kusomewa mashitaka yao mbele ya Hakimu mkazi mkuu Thomas Simba.

Kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 6 ya Mwaka 2021 imesomwa na Wakili wa Serikali Candid Nasua.

Katika shitaka la kwanza Wakili huyo amedai kuwa washitakiwa hao, Januari 13,2021 wakiwa eneo la Magomeni Mwembechai katika Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam walikutwa na meno tisa ya Simba yenye thamani ya Dola za Marekani zaidi ya elfu mbili ni sawa na mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bila kibali cha Mamlaka ya Wanyamapori.

Katika shtaka la pili Wakili Candid amedai kuwa katika tarehe hiyo hiyo eneo la Magomeni Mwembechai jijini Dar es Salaam washitakiwa hao walikutwa na vipande 32 vya meno ya tembo vyenye thamani ya Dola za Marekani elfu kumi na tano mali ya Serikali kinyume na sheria.

Baada ya washitakiwa hao kusomewa mashtaka yao, Hakimu Thomas Simba amedai kuwa hawatakiwi kujibu chochote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi za Uhujumu uchumi.

Aidha Wakili Nasua amedai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika hivyo kuomba mahakama kupanga tarehe nyingine.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Februari 16,2021 kwa ajili ya kutajwa na washitakiwa hao wamerudishwa rumande.