NEMC yaagizwa kutokufanya kazi ya upolisi

0
380

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Ummy Mwalimu ameliagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira nchini kuongeza kasi ya utoaji elimu kwa umma ili kuwasaidia wenye viwanda na wawekezaji kuzingatia Sheria ya Usimamizi wa Mazingira.

Amesema hayo hii leo, Jijini Dodoma alipokuwa akitoa taarifa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Majukumu ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).

Waziri Ummy amesema kumekuwa na malalamiko ya ucheleweshaji wa vibali, utozwaji wa faini kubwa hivyo ameiagiza NEMC kufanya kazi kwa weledi zaidi na kuwaelekeza wawekezaji kufuata taratibu

“NEMC mna kazi ya kuwasaidia wawekezaji kuzingatia sheria na taratibu zilizopo na si vinginevyo, mkiwa wakali watu hawatatii sheria lakini mkielimisha jamii itatii,” amesema Waziri Ummy.

Katika kukabiliana na malalamiko ya wadau kuhusu tozo, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Samuel Gwamaka amesema kuwa kanuni ya ada na tozo za Mazingira ya mwaka 2016, 2018, 2019 imepunguza baadhi ya tozo katika sekta ya kilimo, usajili wa miradi ya tathmini ya athari kwenye mazingira (TAM).

Kwa upande mwingine mjumbe wa kamati hiyo, Askofu Josephat Gwajima ametoa ushauri kwa serikali kubuni miradi ya kuchakata taka ili kuzalisha nishati.

“Ndugu zangu taka hivi sasa ni mali, naishauri serikali kutazama suala hili kwa kina na kuhimiza utenganishaji wa taka kuanzia ngazi ya kaya,” Gwajima amesisitiza.