Halmashauri zatakiwa kuondoa urasimu umilikishaji ardhi

0
384

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi, amezitaka halmashauri zote nchini kupunguza urasimu katika umilikishaji ardhi, kwa sababu wao ndio wasimamizi wa ardhi yote nchini.

Waziri Lukuvi ametoa rai hiyo alipokuwa akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Mwongozo wa Uwekezaji mkoani Iringa, na kuongeza kuwa Mwekezaji yeyote awe wa kutoka ndani au nje ya nchi, cha kwanza anachozingatia ni uwepo wa ardhi.

Akizungumzia Mwongozo huo, Waziri Lukuvi ameupongeza uongozi wa mkoa wa Iringa kwa kuandaa mwongozo huo ambao amesema ni nyaraka ya kwanza yenye taarifa zote za msingi kuwahi kuandaliwa katika ngazi ya mkoa.

Waziri Lukuvi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Isimani lililopo mkoani Iringa, amesema wizara anayoiongoza imerahisisha shughuli za vibali vya ardhi ambapo sasa wameanzisha ofisi mkoani humo, hivyo Wananchi na Wawekezaji hawatahitaji tena kwenda mkoani Mbeya kama ilivyokuwa awali.

Aidha, amewataka Wadau mbalimbali kushirikiana kutekeleza Mwongozo huo, huku akitilia mkazo kuwa, kuandika ni jambo moja, na kutekeleza ni jambo lingine.