Simba kumenyana na TP Mazembe na AL-Hilal

0
231

Klabu ya Simba ya jijini Dar es salaam imetangaza kufanya mashindano maalum yaliyopewa jina la Simba Super Cup, ambayo pamoja na mambo mengine yataikutanisha timu hiyo na timu ya TP Mazembe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na AL-Hilal kutoka nchini Sudan.

Akizungumza na Waandishi wa habari jijini Dar es salaam, Afisa habari wa Simba Haji Manara amesema, mashindano hayo ni sehemu ya kukiandaa kikosi hicho cha Wekundu wa Msimbazi na mashindano ya Klabu Bingwa Barani Afrika.

“Tumeamua kuja na Simba Super Cup kwa kuzialika timu hizi mbili kubwa Barani Afrika ambazo nazo zipo kwenye mashindano makubwa Barani Afrika ili kukijengea kikosi chetu uwezo na kiweze kufika mbali katika mashindano hayo,” amesema Manara.

Kuhusu kocha Mkuu wa timu hiyo, Manara amesema uongozi wa klabu hiyo itamtangaza kabla ya kufanyika kwa mashindano hayo huku akisema kuwa mchezaji wao Benard Morrison ni miongoni mwa wachezaji watakaocheza katika michuano hiyo.

Kuelekea mashindano hayo ya Simba Super Cup
yanayotarajiwa kufanyika Januari 27 mwaka huu katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, Wekundu hao wa Msimbazi wanatarajia kuingia kambini siku ya jumapili ili kujiandaa kuzikabili timu hizo mbili.