Waziri Biteko afanya ziara GST

0
170

Waziri wa Madini Dotto Biteko ameutaka Wakala wa Jiolojia Nchini (GST) kwa kushirikiana na Tume ya Madini kuhakikisha leseni za uchimbaji madini zinazotolewa zinakuwa na taarifa za awali za kijiolojia ili kuwawezesha wachimbaji madini kuchimba wakiwa wanajua ni aina gani ya uchimbaji unapaswa kufanyika katika eneo husika.

Waziri Biteko amesema hayo jijini Dodoma wakati wa mkutano wake na Watendaji wa GST, mara baada ya kufanya ziara katika ofisi za Wakala huo kwa lengo kujua namna unavyotekeleza majukumu yake.

Amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha Wakala.huo unatekeleza majukumu yake ipasavyo na unatoa mchango stahiki katika ukuaji wa sekta ya madini nchini.

Waziri Biteko amesema Serikali imekusudia kuwasaidia Wachimbaji wadogo wa madini kupata taarifa za awali za kijiolojia ambazo pamoja na mambo.mengine zitawasaidia kufanya uchimbaji wa madini unaozingatia utaalamu.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa GST Dkt Mussa Budeba amesema wamepokea maelekezo yote yaliyotolewa na Waziri Biteko.

“Tunashukuru kwa ujio wa Waziri na amezungumza mengi mazuri, yote aliyoagiza sisi kama Wakala tumeanza kuyatekeleza mara baada ya kumalizika kwa mkutano huo,” amesema Dkt Budeba.