Waziri Mkuu amkabidhi nyumba Binti Miriam

0
172

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemkabidhi nyumba ya kuishi binti Miriam Msagati mkazi wa Mombo wilayani Korogwe mkoani Tanga.

Nyumba hiyo ya Miriam ambaye ni mlemavu wa viungo, imejengwa kutokana na michango ya watu mbalimbali wakiongozwa na Waziri Mkuu Majaliwa ambaye alimchangia shilingi milioni 5 alipomtembelea mkoani Tanga mwezi Machi mwaka 2020.

Akikabidhi nyumba hiyo , Waziri Mkuu amesema alimuona binti huyo kupitia kipindi cha Wape Nafasi kinachotangazwa na TBC akimuomba msaada ikiwemo mahali pa kuishi yeye na bibi yake anayemlea Onike Shemdoe.

“Huyu binti nilimuona kwenye kipindi cha TBC, kitu kilichonigusa zaidi ni kwamba aliniomba mimi Waziri Mkuu nimsaidie, kwa kweli kauli yake ilinigusa sana na nikaiweka kichwani nikasema siku nikienda Tanga nitapita,” amesema Waziri Mkuu.

Nyumba hiyo ya Miriam iliyojengwa kwa michango ya watu mbalimbali akiwemo Waziri Mkuu Majaliwa ina mahitaji yote, ambapo Waziri Mkuu amewashukuru wote waliofanikisha ujenzi huo.

“Naomba niwashukuru wote waliofanikisha kukamilisha ujenzi huu, mimi nililichukua hili lakini wengine nao wakaona ni vema washirikiane na mimi kukamilisha ujenzi huu, nawashukuru sana,” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.

Waziri Mkuu amemkabidhi binti Miriam hati ya nyumba hiyo iliyojengwa kwa thamani ya shilingi milioni 47.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa ameendesha harambee kwa ajili ya kukusanya pesa za kumsaidia Miriam kufanya biashara ambapo zaidi ya shilingi milioni 18 zimepatikana.

Kati ya fedha hizo Rais Dkt John Magufuli amechangia shilingi milioni 10 na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amechangia shilingi milioni tano.