Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewahakikishia Wakulima wa zao la mkonge na wafugaji wilayani Korogwe mkoani Tanga mazingira mazuri ya kufanya shughuli zao bila usumbufu wowote.
Waziri Majaliwa ametoa kauli hiyo wakati akipokea taarifa ya maendeleo ya shamba la mifugo la Mruazi lililopo wilayani Korogwe.
Amewashauri Wakulima wa mkonge wilayani Korogwe kulima zao hilo kwa wingi na amewahakikishia upatikanaji wa miche ya zao hilo.
“Twende tukalime mkonge, kulikuwa na siri inafichwa na siri yenyewe ni hili pato ambalo lilikuwa halijulikani, na sisi kama Serikali tunahakikisha miche inapatikana watu walime,” amesisitiza Waziri Mkuu Majaliwa.
Aidha ameziagiza halmashauri zote nchini zinazolima mkonge kutengeneza vitalu vingi kadri ziwezavyo, ili kuwahakikishia Wananchi upatikanaji wa mbegu za kutosha kwa ajili kulima zao hilo.
Kuhusu watu wanaomiliki mashamba makubwa ya mkonge bila kuyaendeleza, Waziri Mkuu Majaliwa amesema Serikali itawanyang’anya na kuyagawa kwa Wananchi wengine ili walime mkonge.
“Tutapata ardhi kupitia mashamba makubwa yaliyotelekezwa na kuyarudisha kwa Wananchi wayaendeleze ili ifikapo mwaka 2025 mavuno yawe yameshamiri tukauze nje. Hivyo nimekuja kwenye kampeni ya kuhamasisha kIlimo cha mkonge kwa sababu ni zao lenye faida nyingi ikiwa ni pamoja na kutengeneza ajira kwa Wananchi,” amesema Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu Majaliwa yuko mkoani Tanga kwa ziara ya kikazi, ziara yenye lengo la kuhawamasisha Wakazi wa mkoa huo kushiriki katika kilimo cha zao la mkonge ili liwaongezee kipato na pia lichangie katika pato la Taifa.