Ujenzi katika shule ya msingi King’ongo kufanyika usiku na mchana

0
186

Uongozi wa mkoa wa Dar es salaam umeanza kutekeleza agizo la Rais Dkt John Magufuli alilolitoa mapem hii leo akiwa mkoani Kagera la kutaka kujengwa kwa madarasa katika shule ya msingi ya King”ongo iliyopo wilayani Ubungo jijini Dar es salaam na kuhakikisha Wanafunzi wa shule hiyo hawakai chini.

Saa chache baada ya Rais Magufuli kutoa agizo hilo Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, – Aboubakar Kunenge alifika shuleni hapo na kuagiza kazi ya ujenzi kuanza mara moja.

Tayari vifaa mbalimbali kwa ajili ya ujenzi wa madarasa hayo vimekwishafikishwa katika eneo husika, na Mkuu huyo wa mkoa ameagiza kazi ya ujenzi kufanyika usiku na mchana chini ya usimamizi wake.

Ameagiza kujengwa kwa vyumba vinane vya madarasa na kubomolewa kwa vyumba vya madarasa ambavyo ni chakavu na kujengwa upya.

Mapema hii leo akizindua shule ya sekondari ya Wavulana ya Ihungo iliyopo mjini Bukoba, Rais Dkt Magufuli aliwaagiza Viongozi wa wilaya ya Ubungo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuhakikisha atakaporejea jijini Dar es salaam, madarasa katika shule hiyo ya msingi ya King’ongo yawe yamekamilika na Wanafunzi hawakai chini