Mvua kubwa yaleta madhara Songea

0
168

Mvua mkubwa iliyoambatana na upepo imesababisha maafa ya kuezuliwa paa katika madarasa matano, ofisi mbili na stoo moja kwenye shule ya msingi ya Mfaranyaki iliyopo manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.

Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa polisi wa mkoa wa Ruvuma, – Simon Maigwa amesema tukio hilo limetokea hii leo majira ya saa tisa mchana, ambapo mvua hiyo imedumu kwa takribani dakika 30.

Kamanda Maigwa amesema licha ya kuezua paa katika madarasa hayo matano, mvua hiyo pia imesababisha madhara kwa kaya tisa ambapo saba ni katika mtaa wa CCM kata ya Mjini na nyumba nyingine mbili za familia za polisi katika kituo kikuu nazo zimeezuliwa paa.

Amesema mvua hiyo pia imeezua paa katika baadhi ya vibanda vya biashara kwenye soko kuu la Songea huku tathmini ya madhara hayo ikiendelea kufanyika.

Diwani wa kata ya Mjini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)katika Manispaa ya Songea Mathew Ngalimanayo amesema hakuna kifo chochote kilichoripotiwa kufuatia mvua hizo.