Serikali ya Zanzibar kuendelea kuwasaidia Wazee

0
141

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Mwinyi amesema Serikali ya awamu ya nane itaendelea kutunga sera na sheria pamoja na kubuni mipango yenye lengo la kuimarisha ustawi wa wazee.

Dkt Mwinyi ameyasema hayo jijini Zanzibar wakati akifungua semina ya mapitio ya utekelezaji wa mradi wa Uwajibikaji na Utimilifu kwa Wazee (Afford II) kwa kipindi cha mwaka 2020 na Mpango wa mwaka 2021.

Amesema Serikali itazingatia mahitaji ya Wazee katika ujenzi wa miundombinu, makazi, pamoja na sekta ya afya na kwamba itaendelea kuimarisha ushirikiano ili kuona kwamba jitihada za kuwatunza wazee zinaleta ufanisi mkubwa zaidi unaokusudiwa.

Kwa mujibu wa Dkt Mwinyi, tayari kuna sheria ya masuala ya Wazee namba 2 ya mwaka 2020 ambayo imeweka utaratibu wa upatikanaji wa haki na huduma za ustawi kwa wazee.

Ameongeza kuwa hatua inayofuata hivi sasa ni kuhakikisha uundwaji wa kanuni za sheria hiyo ili iweze kutumika rasmi na kuiagiza wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Zanzibar iharakishe hatua za kukamilisha kanuni hizo kwa kushirikiana na taasisi husika.