Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Abdallah Ulega
amevitaka vyama na mashirikisho ya michezo nchini kuwa wawazi na wawajibikaji katika matumizi ya fedha za wadhamini, ili kuwapa imani wadau wengi zaidi kuwekeza na kudhamini michezo.
Naibu Waziri Ulega ametoa wito huo jijini Dar es salaam alipokuwa akiwakabidhi zawadi ya udhamini wa masomo wachezaji waliofanya vizuri kwenye ligi ya Taifa ya mpira wa kikapu ya CRDB Bank Taifa Cup 2020.
Aidha Naibu Waziri Ulega ametoa rai kwa benki ya CRDB kudhamini mashindano yajayo ya michezo ya UMISSETA na UMITASHUMTA ili kusaidia katika kuibua vipaji vya vijana shuleni.
Pia ametoa wito kwa Wawekezaji na kampuni mbalimbali kusaidia katika ujenzi wa miundombinu ya michezo hapa nchini, ili vijana wengi waweze kunufaika.
Kupitia udhamini huo, CRDB wamewapatia Wanamichezo 25 takribani shilingi milioni 50 kwa ajili ya kugharamia masomo katika vyuo mbalimbali hapa nchini.